MISINGI YA DA’WAH YA MITUME
MISINGI YA DA’WAH YA MITUME
Misingi yao ni moja
Da’wah ya Mitume yote imewafikiana katika misingi maalumu; msingi wa da’wah ya Mitume ni mmoja, Allah Ta’ala amesema: “Amekuamrisheni Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na tuliyo kufunulia wewe, na tuliyo wausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane kwayo…” (42:13);
Na ndio maana dini ya Mitume yote ikawa ni moja, Allah amesema, “Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na tendeni mema. Hakika Mimi ni Mjuzi wa mnayo yatenda. Na kwa yakini huu Umma wenu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi, basi nicheni Mimi. ” (23:51-52),
Pamoja na sheria zake kutofautiana, Allah amesema, “Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea sharia yake na njia yake” (5:48),
Na lau sheria zingetokea kuwa kinyume na misingi ile basi ingetokea katika hekima, maslahi na huruma, bali ni muhali kuja kinyume na aliyokuja nayo, Allah amesema: “Na lau kuwa Haki ingeli fuata matamanio yao, basi zingeli haribika mbingu na ardhi na waliomo ndani…” (23:71),
Imani na Tawhidi
Na katika kadhia mbalimbali ambazo Mitume wameafikiana na katika ujumbe wake mbali mbali ni:- -Kumuamini Allah, Malaika wake, kitabu chake, Mitume wake, Siku ya Mwisho, na Qadar kheri na shari yake, Allah Mtukuka amesema: “Mtume ameamini yaliyo teremshwa kwake kutoka kwa Mola Mlezi wake, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake na Mitume wake. Hatutafautishi baina ya yeyote katika Mitume wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumet’ii. Tunakutaka maghfira Mola Mlezi wetu! Na marejeo ni kwako.” (2:285).
Amri ya kumuabudu Allah Peke Yake bila ya kumshirikisha yeye na chochote na kumtakasa na kuwa na mke na mtoto, mfano na kuabudu masanamu, Allah Mtukuka amesema: “Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu” (21:25)
Vivyo hivyo amri ya kufuata njia yake, na kutofuata njia tofauti, na kutekeleza ahadi, na kupima sawa sawa kwa kilo na mizani na wema kwa wazazi wawili na uadilifu baina ya watu na ukweli katika kauli na amali, na kuharamisha maovu yaliyodhihiri na yaliyojificha na uovu na kudhulumu, na kuharamisha kuua watoto, na kuua nafsi pasina haki, na kukataza riba na kula mali ya mayatima, na kukataza ubadhirifu na kiburi na kula mali za watu kwa batili. Imani ya siku ya mwisho; kila mtu ana elimu ya yakini kuwa kuna siku ambayo atakufa, lakini nini baada ya kifo chake? Je, ni mwenye furaha au huzuni? Na kila Mitume na Manabii walifikisha na kuwaambia watu wao kuwa watafufuliwa na kulipwa malipo yao, ikiwa kheri basi atalipwa kheri na ikiwa shari atalipwa shari, na jambo hili la kufufuliwa na kuhesabiwa-akili zilizo salimika zinalikubali, na kuungwa mkono na sheria za Mwenyezi Mungu, kwa hakika Muumba mwenye uwezo, mwenye elimu, mwenye hekima ametakasika kuumba viumbe hivi hivi kwa mchezo na bila ya lengo na kuwaacha hivi hivi tu. Allah amesema, “Na hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yao bure. Hiyo ni dhana ya walio kufuru. Ole wao walio kufuru kwa Moto utao wapata.” (38:27)



Comments
Post a Comment