Saumu za Sunna
Maana ya saumu za sunna
Saumu yoyote amabayo sio ya lazima na mtu anaifunga ili kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu U
Na saumu ya sunna ina fadhila kubwa na malipo makubwa. Katika Hadithi Al-Qudsy kutoka kwa Abu Hureirah t Anasema: Amesema Mtume (saw): “Kila kitendo chema cha mwanadamu malipo yake huongezwa, jema moja hulipwa kwa kumi mfano wake mpaka kufikia mara sabini. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Isipokuwa saumu, kwani hiyo ni yangu mimi, na mimi ndiye mwenye kuilipa” [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Siku ambazo kwamba ni sunna kufunga.
1. Siku sita katika mwezi wa Shawwaal (Mfungo mosi)
Kwa kauli ya Mtume (saw): (Atakayefunga Ramadhani, kisha akafuatiliza kwa kufunga siku sita za Shawwaal, itakuwa ni kama aliyefunga mwaka mzima) [Imepokewa na Muslim.].
Sawasawa awe amezifunga siku sita hizi kwa pamoja kufuatana au siku mbalimbali zisizofuatana.
2. Kufunga Siku Tisa za Mwanzo wa Mwezi wa Dhulhijjah. (Mfungo tatu)
Kwa kauli ya Mtume (saw): (Hakuna masiku ambayo matendo mema ni bora zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko masiku haya – yaani masiku kumi ya Dhulhijjah – wakasema (maswahaba): hata jihadi kwa njia ya Mwenyezi Mungu? Akema (Mtume): “Hata jihadi kwa njia ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa mtu aliyetoka (kwenda jihadi) yeye mwenyewe na mali yake, wala asirudi na chochote (yaani akafa vitani)” [Imepokewa na Bukhari.].
Na masiku haya yakatiliwa nguvu zaidi na siku ya A’rafa kando na hajj – nayo ni siku ya tisa ya mwezi wa Dhulhijjah; kwa kauli ya Mtume (saw): (Kufunga siku ya A’rafa nataraji kwa Mwenyezi Mungu kusamehewa mtu madhambi ya mwaka kabla yake, na mwaka uliyo baada yake) [Imepokewa na Muslim.].
3. Kufunga siku ya A’shuura na siku iliyo kabla yake.
Ni siku ya kumi katika mwezi wa Muharam (Mfungo nne).
Kwa kauli ya Mtume (saw): (Na kufunga siku ya A’shuura nataraji kwa Mwenyezi Mungu kusamehewa kwa mtu madhambi ya mwaka uliyo kabla yake) [ Imepokewa na Muslim.].
Na sababu ya kufunga siku hii ni kama ilivyothibiti kutoka kwa Abdillahi ibn Abbas anasema: (Aliingia Madina Mtume (saw) akawaona Mayahudi wamefunga siku ya A’shuura, akasema Mtume: Ni nini hiki (mnachofanya)? Wakasema: Hii ni siku njema, siku hii ndiyo siku Mwenyezi Mungu aliyowaokoa wana israili kutokamana na maadui zao, basi akaifunga siku hii Nabii Musa. Akasema Mtume: Basi mimi nina haki zaidi kwa Musa kuliko nyinyi, akaifunga Mtume siku hiyo na akaamrisha watu kuifunga) [Imepokewa na Bukhari.].
Na inapendekezwa vile vile kufunga siku ya tisa, kwa ilivyo pokelewa kutoka kwa Mtume (saw) Alisema (Lau nitaishi mpaka Mwaka ujao nitafunga siku ya tisa) [ Imepokewa na Muslim.]
4. Kufunga Masiku meupe ya kila mwezi
Nayo ni tarehe kumi na tatu, na kumi na nne, na kumi na tano ya kila mwezi katika miezi ya kiislamu, na yameitwa meupe; kwasababu usiku wa masiku haya hunga’ra kwa mwangaza wa mwezi.
Kama ilivyothibiti kutoka kwa AbdulMalik ibn Minhal kutoka kwa babake: Kwamba (babake) alikuwa pamoja na Mtume (saw) akasema (kumwambia mwanaye – AbdulMalik): Alikuwa Mtume (saw) akiwaamrisha kufunga masiku meupe, na akisema: (Masiku) haya ni saumu za mwaka) [Imepokewa na Ibnu Hibbaan.]
5. kufunga siku mbili – jumatatu na alhamisi katika kila wiki.
Kama ilivyopokewa kutoka kwa Abu Hureira t kwamba Mtume ﷺ amesema: “Hupandishwa matendo (juu kwenda mbinguni) kila jumatatu na alhamisi, basi napenda matendo yangu yapandishwe hali ya kuwa nimefunga” [Imepokewa na Tirmidhi.].
6. Kufunga siku Moja na kula siku Nyingine
Bora katika funga za sunnah ni saumu ya Nabii Daud juu yake iwe amani – Alikuwa akifunga siku moja na kuacha siku moja; kutoka kwa Abdillahi ibn A’mru t Anasema: Amesema Mtume (saw): (Hakika saumu ya kupendeza sana mbele ya Mwenyezi Mungu ni saumu ya Daud, na alikuwa akifunga siku moja na kula siku moja) [Imepokewa na Nasaai.].



Comments
Post a Comment