Tarekh ya mitume:Mohammad
Tarekh ya mitume:Mohammad
Bishara ya Mtume wa mwisho
Mtume Muhammad (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) ni mwisho wa mitume na manabii, Issa – (‘Alayhi salaam) amewabashiria Bani Israil kuja mtume wa mwisho, Allah amesema: “Na Isa bin Mariamu alipo sema: Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninaye thibitisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria kuja Mtume atakaye kuja baada yangu; jina lake ni Ahmad! Lakini alipo waletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhaahiri!” (61:6),
Hivyo basi bishara ya Mtume (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) ipo katika Taurati na Injili. Allah amesema: “Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiye soma wala kuandika, wanaye mkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anaye waamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na ana waharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyo kuwa juu yao. Basi wale walio muamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyo teremshwa pamoja naye - hao ndio wenye kufanikiwa.” (7:157),
Bali Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) amechukua ahadi na mkataba kwa manabii wamuamini Muhammad (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam) na wamnusuru yeye kama atatumwa kwao wakiwa hai, na wawaambie kaumu zao hilo ili habari yenyewe ienee baina ya Ummah zote, Allah amesema: “Na pale Mwenyezi Mungu alipo chukua ahadi kwa Manabii: Nikisha kupeni Kitabu na hikima, kisha akakujieni Mtume mwenye kusadikisha mliyo nayo, ni juu yenu mumuamini na mumsaidie. Akasema: Je, mmekiri na mmekubali kushika agizo langu juu ya hayo? Wakasema: Tumekubali. Akasema: Basi shuhudieni, na Mimi ni pamoja nanyi katika kushuhudia.” (3:81)
Qur-aan imeashiria bishara hizo, na kuthibitisha ukweli wa Muhammad (Swala Llahu ‘alayhi wasalaam), Allah amesema: “Na walio kufuru wanasema: Wewe hukutumwa. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi, na pia yule mwenye ilimu ya Kitabu” (13:43),
Na katika aya nyingine: “Na hakika bila ya shaka haya yamo katika Vitabu vya kale. Je! Haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanazuoni wa Wana wa Israili? ” (26:196-197)
Na akazungumzia kuhusu msimamo wa Ahlul kitab ambao ilipasa kuwa ndio wa mwanzo na waumini kwa kumjua kwao kama walivyokuwa wakiwajua watoto wao: “Wale tulio wapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyo wajua watoto wao; na kuna kikundi katika wao huificha haki na hali wanajua.” (2:146),
Allah Mtukuka amesema: “Na alipo wajia Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwenye kuthibitisha yale waliyo nayo, kundi moja miongoni mwa wale walio pewa Kitabu lilitupa Kitabu cha Mwenyezi Mungu hicho nyuma ya migongo yao kama kwamba hawajui.” (2:101),


Comments
Post a Comment