Tarekh ya mitume:Nuuh

Kaumu ya Nuhu

Watu wake hapo kabla walikuwa ni waumini, wakimuabudu Allah peke yake, wakiamini Siku ya Mwisho, na wakifanya mambo mema, watu wale akafa, watu wakahuzunika kwa wema wao na tabia zao njema wakatengeneza picha zao (Wakawapa majina yafuatayo: Wadda, Yaaghutha,Yaa’uqa, Nasra, watu wakavutika na picha zile na…) wakafanya ndio alama za wale watu wema waliokufa miongoni mwao, watu wa mjini wakatukuza picha zile, wakikusudia kuwatukuza wafu wale muda ukapita wale watu wazima wakafa na kubaki watoto na kuwa wakubwa, wakawa wanaongezea namna mbali mbali za kutukuza, na kunyenyekea mbele zao, picha na sura zile zikawa na nafasi kubwa katika mioyo ya watu wale, ama kizazi cha pili kilichofuatia wakawa wamejiwekea sheria ya kuabudu sura zile na kusema kuwa ile ni miungu inabidi wayasujudie na kunyenyekea mbele yake; wakawa wanayaabudu, wengi wakapotea kwa kufanya hivyo.
Baada ya hapo Allah akawatumia watu wale Mtume Nuhu (‘Alahyi Salaam); ili awaelekeze njia (iliyonyooka), na kuwakataza kuabudu masanamu, na kuwaelekeza kumuabudu Allah Ta’ala, Nuhu (‘Alahyi Salaam) akaenda kwa kaumu yake… “…Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu asiye kuwa Yeye…” (23:23)
Wakamkadhibisha, na hawakumkubali, akawaonya na kuwatahadharisha adhabu ya Allah Ta’ala. Akasema: “Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Kubwa.” (26:135),
Wakasema: “Wale watukufu katika kaumu yake wakasema: Hakika sisi tunakuona wewe umo katika upotofu ulio dhaahiri.” (7:60),
Nuhu akawajibu: “Akasema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika upotofu, lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote. Nakufikishieni Ujumbe wa Mola Mlezi wangu, na ninakunasihini; na ninayajua kwa Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi.” (7:61-62)
Watu wakashangazwa na maneno ya Nuhu, wakawa wanasema. Wewe ni mtu kama sisi, utakuwaje Mtume kutoka kwa Allah? Na ambao wamekufuata ni kundi la watu dhaifu na watu wa chini, kisha hamna ubora kutushinda sisi, si katika mali wala katika vyeo, na sisi tunadhania kuwa mnadanganya katika madai yenu haya, baadhi ya kaumu wakawaambia wengine: “…Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi. Anataka kujipa ubora juu yenu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu amependa basi yakini angeli teremsha Malaika. Hatukusikia haya kwa baba zetu wa zamani. Huyu si lolote ila ni mtu mwenye wazimu…” (23:24-25)
Baadhi yao wakahamasisha wengine kuabudu masanamu yao: “Na wakasema: Msiwaache miungu yenu, wala msimwache Wadda wala Suwaa’ wala Yaghutha, wala Yau’qa, wala Nasra. ” (71:23).
Nuhu (‘Alayhi salaam) akawaambia: “Je, mnastaajabu kukujieni mawaidha yanayotoka kwa Mola Mlezi wenu kwa njia ya mtu aliye ni mmoja katika nyinyi, ili akuonyeni…” (7:63)
Na baada ya hapo Nuhu akawachukulia kwa upole na ulaini, lakini watu waliendelea na inadi yao, na akawalingania wakati wote mpaka akasema: “Akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimewaita watu wangu usiku na mchana, Lakini wito wangu haukuwazidisha ila kukimbia. Na hakika mimi kila nilipo waita ili upate kuwaghufiria, walijiziba masikio yao kwa vidole vyao, na wakajigubika nguo zao, na wakakamia, na wakatakabari vikubwa mno! ” (71:5-7)
Akawalingania katika kila njia iliyowezekana: “Tena niliwaita kwa uwazi, Kisha nikawatangazia kwa kelele, tena nikasema nao kwa siri.” (71: 9-10),
Wengine wakajiundia nyudhuru duni kwa kusema: “Wakasema: Je! Tukuamini wewe, hali wanao kufuata ni watu wa chini?” (26:111)

Comments

Popular Posts