Tarekh ya mitume:utangulizi mkuu

Tarekh ya mitume:utangulizi mkuu

Imani kwa mitume

Watu walikuwa katika uongofu na wakatofautiana, Allah akatuma Mitume, ili awafundishe watu na awaonye:“Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri” (62:2)
Lakini watu wakagawanyika kulingana na da’wah ya Mitume katika makundi mawili; kundi lililokubali (lililosadikisha) Mitume na kuamini, na kundi lililokadhibisha Mitume na kuwakana na kile walichokuja nacho, waliwakadhibisha kwa ujeuri; “Watu wote wa likuwa ni umma mmoja. Mwenyezi Mungu akapeleka Manabii wabashiri na waonyaji. Na pamoja nao akateremsha Kitabu kwa Haki, ili kihukumu baina ya watu katika yale walio khitalifiana. Na wala hawakukhitalifiana ila wale walio pewa Kitabu hicho baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi, kwa sababu ya uhasidi baina yao. Ndipo Mwenyezi Mungu kwa idhini yake akawaongoa walio amini kwendea haki katika mambo waliyo khitalifiana. Na Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.” (2:213)
Na walikadhibisha kwa kiburi na kufuata matamanio yao, “…Basi kila walipo kufikieni Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha, na wengine mkawauwa.” (2:87).
Allah Ta’ala ameamrisha Mitume wote waaminiwe, “Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyo teremshiwa sisi, na yaliyo teremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na wajukuu zake, na waliyo pewa Musa na Isa, na pia waliyo pewa Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi tumesilimu kwake.” (2:136),
Na akawaahidi watakaoamini Mitume kupata furaha, na uokozi hapa duniani na akhera, na akawakamia watakaokufuru na kuupa mgongo kupata khasara na tabu hapa duniani kabla ya kesho akhera, Allah amesema,“Na atakaye fanya urafiki na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walio amini, basi hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kushinda.” (5:56)
Na akasema vile vile:“Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua! Wale walio amini na wakatenda mema watakuwa na raha na marejeo mazuri.” (13:28-29)

Comments

Popular Posts